Search This Blog

Thursday, June 7, 2012

CHANGAMOTO ZA WANAFUNZI WA AFRIKA WANAOSOMA ULAYA


CHANGAMOTO ZA WANAFUNZI WA AFRIKA WANAOSOMA ULAYAImekuwa ikijulikana enzi na enzi, lakini pia ndio ukweli mambo na wahenga waliwahi kunena kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha. Msemo huu ni sahihi kabisa kwani elimu ndio chanzo kikubwa cha kuweza kuwaamsha watu na kuweza kuwapa uwezo wa kuona mambo mbalimbali katika mitazamo na upeo mkubwa. Elimu nzuri imekuwa ikiwasadia watu kupambanua matatizo mbalimbali na kuyatafutia fumbuzi mbali mbali ambazo zikitumika na zikitumiwa kulingana na ushauri wa wasomi na wataalamu zinatatua matatizo mbalimbali ya jamii inayowazunguka wahusika.

Kwa umuhimu wa elimu katika jamii zetu na ulimwengu wote kwa ujumla, watu wamekuwa wakiitafuta hii bidhaa “Elimu” kwa udi na uvumba. Haijalisha inapatika wapi, cha msingi aipate hii bidhaa katika ubora wake ili baadae mtu huyu afaidike nayo binafsi na jamii yake kwa ujumla. Katika kuitafuta elimu bora, kumekuwa na wimbi kubwa la vijana toka Afrika kuitafuta elimu katika nchi za Ulaya, Marekani na Asia kwa kile kinachoaminika huko watapata elimu bora na si bora elimu.
Katika kuitafuta elimu, vijana wengi wa kiafrika wanaosoma nchi za magharibi, Marekani na Asia wamekuwa wakipitia changamoto nyingi tangu mwanzo wa safari yao ya utafutaji wa elimu hadi kukamilisha. Kazi hii ya utafutaji wa elimu si rahisi.

Changamoto ya kwanza kabisa wanayokumbana nayo wapiganaji wanaotafuta elimu, ni elimu hii kuwa ya gharama kubwa sana katika nchi hizi kiasi kwamba watu wachache sana toka afrika wanaoweza kujilipia gharama zote za shule huko kunakoitwa “majuu”. Hivyo wengi wa vijana toka Afrika huhangaikia upatikanaji wa ufadhili toka mataifa hayo hayo yenye elimu bora. Kwa bahati mbaya sana nafasi za ufadhili huwa chache sana. Hivyo basi, idadi ya waombaji huwa kubwa sana kulinganasha na idadi ya nafasi zinazotolewa. Hivyo changamoto ya mchujo huwakumba wengi na walio wengi hukosa ufadhili kulinganisha na wanaopata. Utakuta hata ambao wamepata, walikuwa wakiomba ufadhili hata kwa miaka miwili, mitatu wengine hadi minne hata mitano mfulizo ndio wanapata ufadhili.

Wanaokosa kwa kipindi walichoomba, wanashauriwa kutokata tamaa na kuomba kwa msimu unaofutia tena na tena. Sasa kwa wale wanaobahatika kupata ufadhili na kufanikiwa kwenda nchi za ugenini wanakumbana na changamoto nyingine nyingi wakiwa huko. Mabadiliko ya hali ya hewa si jambo la kubeza hata kidogo. Kuna tofauti kubwa sana ya hali ya hewa kwa mfano nchi za Scandinavia na Afrika kwa ujumla ni tofauti kubwa sana. Hali ya hewa kwa Afrika kwa ujumla ni joto, na baridi si kitu cha kawaida sana kwa nchi nyingi za Afrika hasa Afrika mashariki. Sasa kwa nchi za Scandinavia baridi huenda hadi jotoridi la nyuzi hasi 30 (-30˚C). Hii sio baridi ya kawaida ukiongezea na barafu kubwa ambalo huwa linatanda katika kila sehemu kwa mtu aliyezoea joto. Ni mateso makubwa, bila uvumilivu ni ngumu sana kudumu katika hali kama hii.

Utamaduni wa chi nyingi za magharibi ni tofauti kabisa na utamaduni wa chi za Afrika. Hii nayo huwa ni changamoto kubwa kwa wanafunzi wanaosoma katika nchi za magharibi. Tukiwa Afrika, tumezoea kuwaona ndugu wa magharibi kwenye luninga zetu na kudhani mambo wanayofanya ni mambo ya tamthiliya. Sasa wanaobahatika kuishi nao wanajionea mengi. Mambo ambayo kwetu Afrika hayafanywi hadharani, basi ndugu wa magharibi wanayafanya hadharani bila woga wala aibu yoyote. Hili ni gumzo kubwa sana kwa vijana wanaosoma katika vyuo vya mataifa ya magharibi. Mambo ya kutokuwa na imani kwa Mungu nayo ni changamoto kwa waafrika walio wengi maana huja na imani zao huku magharibi. Sasa wakifiki huku wenzao wa magharibi wanaanza kuwashangaa na kuwaona wamepitwa na wakati na wanapoteza muda kumwamini Mungu. Sasa kama mwafrika hajaishika vizuri imani yake, ni rahisi sana kuiacha na kufuata wanavyofanya wazungu. Nimeona baadhi ya mabinti ambao wamekuwa wepesi kuiga tamaduni za huku magharibi na kuishi kama hawa ndugu wa magharibi wanavyoishi. Sijui ni kwa nini inakuwa rahisi sana kwa dada zetu kubadilika kwa urahisi namna hii. Hii inatokea pia kwa vijana ingawaje mara chache sana. Utawakuta baadhi ya vijana nao wanaiga kutoboa masikio na pua na kuvaa urembo kama wanawake. Hii ni changamoto kubwa kwa wanafunzi wa kiafrika.

Suala la technolojia limekuwa pia changamoto kubwa hasa siku za mwanzoni za maisha ya waafika katika mataifa ya magharibi. Kila kitu kinaendeshwa kwa mfumo wa kompyuta. Ni kitu kigeni sana kwa wanafunzi walio wengi wanaotoka afrika, maana wengi wao hawajazoea mfumo huu wa elimu. Kila matangazo na taarifa nyeti zipo kwenye mtandao wa kumpyuta. Sasa waafrika wengi wanapitwa na mambo na taarifa za muhimu hasa siku za mwanzoni kwani wanakuwa hawajazoea mfumo huu wa elimu na upashanaji habari. Na mbaya zaidi wanafunzi na watu wote wa magharibi kwa ujumla, hawana utamaduni wa kujulishana na kupashana habari kwa kile kinachoendelea, kila mtu kivyake vyake tu. Mzungu anaweza kumwona mwenzake amepotea njia na asimwambie kuwa amepotea. Ni tofauti sana na nchi nyingi za kiafrika ambako utamaduni wa kupashana habari na kusaidiana ndio jadi yetu.  Gharama ya maisha kuwa juu sana ni changamoto nyingine ambayo imekuwa ikiwakumba waafrika wengi wanaosoma nchi za magharibi. Gharama za maisha ziko juu sana, kuanzia upangaji wa nyumba, vyakula, usafiri na vinginevyo vingi viko juu sana. Usipokuwa makini hela yote unayopata kwa ufadhili inaweza kuisha na ukabaki unaishi maisha magumu sana. Hivyo yatakiwa kuwa makini sana katika kupanga matumizi yako ili hela unayopata iweze kukusaidia kukufikisha mwisho wa masomo.
Kuna changamoto nyingine nyingi kulingana na mazingira mtu anayoishi na hali yake alivyoiacha huko nyumbani kwao afrika. Kuna baadhi ya watu wanaishi maisha tofauti kabisa ingawaje hela ya ufadhili wanayopata ni sawa kabisa. Sasa hili na mengine tutaendelea kujadiliana katika makala zinazofuata. Cha msingi kujua na kujifunza kutokana na hizi changamoto ni kuwa, tunaziweka wazi hivi ili mtu akiwa anajiandaa kuja kusoma nchi za magharibi ajiandae kiakili na kisaikolojia kabla hajafika huku magharibi, ili pindi akifika huku magharibi asije akashangazwa na yale na atakayoyakuta na kuyaona. Hii itayafanya maisha yake ughaibuni kutokuwa magumu sana kwani tayari anajua atakachokuja kupambana nacho. Pia kuna faida nyingi sana za kujipatia elimu toka mataifa ya magharibi pamoja na kuishi huku. Yapo mengi sana ya kujifunza ambayo ukiyachukua kwa mtazamo chanya yanaweza kuwa chachu nzuri ya mabadiliko ya bara letu la Afrika ambalo bado liko nyuma sana kimaendeleo ya sayansi na technolojia. Haya na mengine mengi yatawajia katika makala nyingi zinazofuata, ambazo tutajadili mengi kuhusiana na maisha ya wanafunzi wa kiafrika wanaosoma katika vyuo vya mataifa ya magharibi. Usikose makala zifuatazo.

PETER MAKOLO
MSc. In Electric Power Engineering
Chalmers University of Technology (CTH)
G├Âteborg, SWEDEN
+46 739 635 772
 


1 comment:

Lusasi said...

Ni changamoto zenye changamoto.Ideally wanafunzi wa kibongo tulitakiwa kutambuliwa na serikali zetu kuwa tuko masomoni kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu,hivyo tukwamapo basi nchi zetu ndo zingepunguza ugumu wa maisha na sio nchi kuchukua jukumu la kutangaza misiba pale wenzetu wenye roho nyepesi wanaposhindwa kuvumilia magumu ya maisha wakiwa majuu.lets think big to overcome the obstacles.